Wakimbizi kutoka Ethiopia waendelea kumiminika Sudan
(last modified Wed, 06 Jan 2021 08:20:33 GMT )
Jan 06, 2021 08:20 UTC
  • Wakimbizi kutoka Ethiopia waendelea kumiminika Sudan

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR linaendelea kuandikisha wakimbizi wapya katika mpaka wa Sudan na Ethiopia ambapo takriban wakimbizi 800 wamevuka kutoka eneo la Tigray nchini Ethiopia na kuingia mashariki mwa Sudan katika siku chache za mwaka huu wa 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu, mjini Geneva Uswis, msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic amesema tangu Novemba mwaka jana, zaidi ya wakimbizi 56,000 kutoka Ethiopia wamefungasha virago kukimbia machafuko na kuingia nchi jirani Sudan na kwamba,“Wanaowasili wanaelezea kuwa katikati ya mzozo na kuwa waathirika wa makundi kadhaa yaliyojihami huku wakikabiliwa na hali ngumu ikiwemo, uporaji wa nyumba zao, kutumikishwa kwa lazima kwa wanaume na wavulana, na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana.”

UNHCR imesema wakimbizi wanaowasili wanafika na nguo tu walizovaa, wakiwa wamechoka na wakiwa dhaifu baada ya safari ya siku nyingi. Asilimia 30 ya  wakimbizi wanatajwa kuwa chini ya umri wa miaka 18 na asilimia 5 wana umri wa zaidi ya miaka 60.

Mahecic ameongeza kwamba kwa kushirikiana na serikali ya Sudan, UNHCR na kamisheni ya wakimbizi Sudan, COR wanaendelea kuhamisha wakimbizi kutoka kwenye maeneo ya mapokezi ambayo yamejaa hadi kwenye kambi zilizoko jimbo la Gedaref. Aidha amesema mahitaji ya wakimbizi ni mengi na kwamba,“Serikali ya Sudan inaendelea kuacha mipaka yake wazi kwa ajili ya wakimbizi lakini msaada zaidi unahitajika hususan kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji na kujisafi kwenye kambi na maeneo ya mapokezi. Pia kuimarisha mbinu za kuzuia Covid-19 ikiwemo kujitenga.”

Mapigano yanaripotiwa kuendelea katika mkoa wa Tigray, karibu miezi miwili sasa baada ya kuzuka kwa mapigano katika jimbo hilo linalotaka kujitenga.

Serikali ya Ethiopia inasisitiza kuwa hali ni shwari katika mkoa wa Tigray, lakini ni vigumu kuingia katika jimbo hilo Tigray.

Hata hivyo misafara ya magari ya mashirika ya misaada ya kibinadamu imeendelea kuingiza misaada ya chakula ingawa hali bado ni tete na mawasiliano mpaka sasa yamekatwa.

Vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray ya TPLF pia vinaendelea na vita, kutoka maeneo ya vijijini.

Wakati jeshi la Ethiopia linadhibiti makao makuu ya jimbo la Tigray, hofu  inaendelea katika vijiji vya jimbo hilo.

Eneo la Tigray lililoko kaskazini ya Ethiopia limeshuhudia mapigano katika wiki za karibuni kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF.

Serikali ya Adds Ababa, ambayo inaituhumu TPLF kuwa inataka kulitenganisha eneo la Tigray na ardhi ya Ethiopia, lilitangaza hivi karibuni kuwa vikosi vya jeshi vimeudhibiti mji wa Mekelle, makao makuu ya eneo hilo.

 

Tags