Corona imeua wanahabari 28 barani Afrika tokea Machi 2020
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65626-corona_imeua_wanahabari_28_barani_afrika_tokea_machi_2020
Shirika moja la kufuatilia maslahi ya waandishi wa habari la Uswisi limesema jumla ya waandishi wa habari 600 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 kote duniani tokea mwezi Machi mwaka uliomalizika 2020 hadi sasa, ambapo 28 miongoni mwao ni wa nchi za Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2021 23:07 UTC
  • Corona imeua wanahabari 28 barani Afrika tokea Machi 2020

Shirika moja la kufuatilia maslahi ya waandishi wa habari la Uswisi limesema jumla ya waandishi wa habari 600 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 kote duniani tokea mwezi Machi mwaka uliomalizika 2020 hadi sasa, ambapo 28 miongoni mwao ni wa nchi za Afrika.

Shirika hilo la Press Emblem Campaign (PEC) limesema katika ripoti yake mpya kuwa, Amerika ya Latini inaongoza kwa vifo hivyo, ambapo wanahabari 303 waliaga dunia katika kanda hiyo. Bara la Asia linafuata kwa vifo 145 mbele ya bara Ulaya lililoripoti vifo 94.

Amerika Kaskazini imeripoti vifo vya wanahabari 32 kutokana na ugonjwa wa Covid-91 tokea mwezi Machi mwaka jana hadi sasa, huku bara la Afrika likifunga orodha hiyo kwa vifo 28.

Peru ndiyo nchi iliyosajili vifo vingi vya waandishi wa habari kutokana na janga la corona, ambapo wanahabari 93 wameaga dunia katika kipindi hicho tajwa kwa mujibu wa Chama cha Kitaifa cha Wanahabari cha Peru (Peruvian National Association of Journalists), ikifuatia na Brazil vifo 55, India 53, Mexico 45, Ecuador 42 na Bangladesh 41.

Wanahabari kazini

Blaise Lempen, Katibu Mkuu wa shirika la Press Emblem Campaign (PEC) amesema kuwa, waandishi wa habari wanapaswa kupewa kipaumbele katika kampeni ya kupigwa chanjo ya corona inayoendelea katika maeneo mbalimbali duniani.

Amebainisha kuwa: Kutokana na taaluma yao, wanahabari wanaoenda nyanjani kutafuta na kupashana habari wapo katika hatari ya kukumbwa na virusi vya corona. Baadhi yao hususan wanahabari binafsi na wapigapicha hawawezi kufanyia kazi zao nyumbani, sharti watoke nje. Kwa msingi huo wanapaswa kuzingatiwa katika utoaji wa chanjo za kukabiliana na corona.