Vifo na kunyongwa wafungwa katika magereza ya Misri vyaongezeka
Kitengo cha upashaji habari cha Misri kimetangaza kuwa watuhumiwa wa masuala ya kisiasa wasiopungua 37 walinyongwa mwaka uliopita wa 2020 na watu wengine 75 waliaga dunia kwa uzembe wa kutopatiwa matibabu katika magereza ya Misri.
Kitengo hicho kimetoa ripoti yake chini ya anwani "Rekodi Nyeusi ya Utawala wa Abdel Fattah al Sisi katika mwaka 2020" na kueleza kuwa: Tangu mwanzoni mwa mwaka 2020 mauaji ya uhalifu na ya kisiasa yaliongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini Misri.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, katika kipindi cha miezi ya Oktoba na Novemba mwaka jana pekee watu 57 ama walinyongwa au waliaga dunia katika magereza za Misri kwa uzembe wa kutopatiwa matibabu; idadi ambayo ni mara mbili ya ile ya walionyongwa mwaka 2019.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa: Al Sisi anawashinikiza wapinzani wake na kuzitia mbaroni familia zao ili kuwanyamazisha. Hii ni katika hali ambayo ndugu kadhaa wa familia hizo za wapinzani nchini Misri wameaga dunia magerezani.
Kitengo cha upashaji habari cha Misri kimeutaja mwaka jana wa 2020 kuwa ulioshuhudia wimbi kubwa la vitendo vya ulipizaji kisasi dhidi ya wafungwa hususan katika jela ya al Aqrab ambayo sasa imegeuzwa na kuwa kaburi la watu hai.
Kwa mara ya kwanza mwezi Juni mwaka 2012 wananchi wa Misri walishiriki katika uchaguzi wa kwanza wa Rais uliofanyika kwa njia ya kidemokrasia na kumchagua mwendazake Muhammad Morsi kuwa rais wa nchi baada ya kumng'oa madarakani dikteta wa nchi hiyo Hosni Mubarak katika mapinduzi ya mwezi Januari.
Hata hivyo Morsi aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 3 Julai 2013 yaliyoongozwa na waziri wa ulinzi wakati huo Jenerali Abdel Fattah el Sisi. Baada ya kuondolewa madarakani rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, viongozi wote waandamizi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin akiwemo Morsi mwenyewe, walikamatwa na kutiwa gerezani.