Misri yawaweka viongozi 50 wa Ikhwanul Muslimin katika orodha ya magaidi
(last modified Tue, 26 Jan 2021 10:55:36 GMT )
Jan 26, 2021 10:55 UTC
  • Misri yawaweka viongozi 50 wa Ikhwanul Muslimin katika orodha ya magaidi

Mahakama nchini Misri imewaweka viongozi 50 wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo katika orodha ya magaidi.

 Abdulmun'im Abulfutuh, Mahmouda Izzat, Hassan Malik na Omar al-Saidi ni miongoni mwa viongozi ambao majina yao yamewekwa katika orodha hiyo ya makundi ya kigaidi.

Mahakama hiyo ya mjini Cairo imedai kuwa: Uamuzi huo umetolewa katika fremu ya mpango wa kupambana na aina mbalimbali za ugaidi na kwamba kuwepo watu hao kunaitishia Misri, raia wake, haki na uhuru wa wananchi.  

Kadhalika mahakama hiyo ya Misri imerefusha kwa muda wa miaka mitano mingine, uamuzi wake wa kuiarifisha Harakati ya Ikwanul Muslimin kama kundi la kigaidi. Harakati hiyo ya Kiislamu ilitangazwa kuwa kundi la kigaidi kwa mara ya kwanza mwaka 2013.

Baada ya jeshi la Misri likiongozwa na Waziri wa Ulinzi Jenerali Abdel Fattah al-Sisi kufanya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Mohammad Morsi mnamo tarehe 3 Julai 2013 na kuondolewa madarakani rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo, viongozi wote waandamizi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin akiwemo Morsi mwenyewe walikamatwa na kutiwa gerezani.

Nembo ya Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri

Tangu wakati huo hadi sasa, mahakama za Misri chini ya utawala wa al-Sisi zimeshatoa hukumu za vifo, vifungo vya maisha jela na vya miaka kadhaa kwa viongozi na wanachama wengi waandamizi wa Ikhwanul Muslimin. 

Morsi, aliaga dunia tarehe 17 Juni 2019 baada ya kuanguka mahakamani alikofikishwa kujibu moja ya kesi zilizokuwa zikimkabili.

Tags