Kaburi la umati la Waislamu wa Zaria lagunduliwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i664-kaburi_la_umati_la_waislamu_wa_zaria_lagunduliwa_nigeria
Wanaharakati wa Nigeria wamegundua kaburi la umati la Waislamu waliouawa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Zaria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2016 12:36 UTC
  • Kaburi la umati la Waislamu wa Zaria lagunduliwa Nigeria

Wanaharakati wa Nigeria wamegundua kaburi la umati la Waislamu waliouawa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Zaria.

Ripoti zinasema kuwa wanaharakati wa Nigeria leo Ijumaa wametangaza kuwa kaburi hilo lililogunduliwa katika makaburi ya Mando Kaduna ni moja ya makaburi ya umati ambamo jeshi la Nigeria lilizika zaidi ya maiti za Waislamu 1000 wa mji wa Zaria.

Shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria mwezi mwezi Disemba dhidi ya Waislamu wa mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna bado linazungumziwa kwa wingi katika duru mbalimbali na maafa hayo makubwa yamelaaniwa na mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu likiwemo lile la Human Rights Watch.

Tarehe 12 hadi 14 Disemba jeshi la Nigeria lilishambulia kituo cha kidini na nyumba ya kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mji wa Zaria na kuua mamia ya Waislamu wasio na hatia. Sheikh Zakzaky ambaye alipigwa risasi kadhaa katika hujuma hiyo na mamia ya Waislamu wengine bado wanashikiliwa na jeshi la Nigeria sehemu isiyojulikana.