AU yashtushwa na machafuko ya baada ya uchaguzi CAR
Umoja wa Afrika umeeleza wasi wasi wake kutokana na kushtadi machafuko ya baada ya uchaguzi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na AU imesema kuwa: Kikao cha hivi punde cha Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika kimeeleza kusikitishwa na machafuko ya baada ya uchaguzi wa hivi karibuni yanayoendelea kushuhudiwa, na ambayo yamekwamisha kufikiwa na misaada ya kibinadamu wakimbizi wa ndani waliofurushwa makwao kutokana na ghasia hizo.
Taarifa hiyo ya AU sambamba na kutoa mwito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa yatakayojumuisha makundi yote ya kisiasa, imeyataka makundi yanayobeba silaha hususan yanayoongozwa na rais wa zamani, Francois Bozize yasichukue hatua yoyote inayoweza kushadidisha hali ya taharuki na machafuko nchini humo.
Kikao hicho cha Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika kimesema watakaokiuka makubaliano ya amani na maridhiano baina ya serikali na makundi ya waasi (APPR-CAR) watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), watu zaidi ya 200,000 wamefurushwa au wamelazimika kuyahama makazi yao katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kutokana na machafuko ya uchaguzi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ghasia hizo za uchaguzi zilishtadi baada ya Rais Faustin-Archange Touadera wa nchi hiyo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa mwishoni mwa mwezi Disemba 2020, kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi wa duru moja na hivyo kukwepa kuingia katika uchaguzi mwingine.
Januari 18, Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo iliidhinisha ushindi huo wa Toudera wa uchaguzi wa rais wa Disemba 27.