Mawaziri watatu wakumbwa na ugonjwa wa corona nchini Misri
Mawaziri watatu wa Misri yaani waziri wa biashara na viwanda, waziri wa mahakama na waziri wa fedha wamekumbwa na ugonjwa wa COVID-19.
Shirika la habari la FARS limenukuu taarifa ya wizara ya viwanda ya Misri ikithibitisha habari hiyo na kusisitiza kuwa, mawaziri wote hao watatu wamepatwa na ugonjwa wa corona ambao majina yao kwa utaratibu ni Niflin Jamii, Amr Marwan na Muhammad Muit.
Hata hivyo hadi tunapokea habari hii, serikali ya Misri ilikuwa bado haijathibitisha habari hiyo.
Mwezi Juni mwaka jana 2020 pia, Usamah Haikal, waziri wa habari wa Misri naye alikumbwa na ugonjwa wa COVID-19 na baadaye akapata afueni baada ya kupita takriban wiki mbili.
Hadi leo mchana, idadi ya watu waliokuwa wameshakumbwa na ugonjwa wa corona nchini Misri walikuwa wameshafikia 178,151. Kati ya hao, 10,353 walikuwa wameshafariki dunia na karibu laki moja na 37,837 walikuwa wameshapa afueni na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Ukitoa Afrika Kusini, Morocco na Tunisia; Misri ni ya nne barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa corona kwa mujibu wa mtandao wa worldometers unaotoa takwimu mubashara za wagonjwa wa COVID-19.
Hadi leo mchana idadi ya watu wote waliothibitishwa kukumbwa na ugonjwa wa corona duniani walikuwa ni 112,024,400. Waliofariki dunia kwa ugonjwa huo walikuwa wameshafikia 2,479,255 na waliopata afueni walikuwa ni 87,390,705 katika kona mbalimbali za dunia.