Makumi wapoteza maisha baada ya treni mbili kugongana Misri
(last modified Sat, 27 Mar 2021 03:03:17 GMT )
Mar 27, 2021 03:03 UTC
  • Makumi wapoteza maisha baada ya treni mbili kugongana Misri

Makumi ya watu wameaga dunia huku wengine wengi wakijeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea kusini mwa Misri.

Ripoti zinasema watu wasiopungua 32 wamefariki dunia katika ajali hiyo ya jana Ijumaa, huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa. 

Idara ya Usafiri wa Garimoshi ya Misri imetangaza kuwa, ajali hiyo imetokea baada ya treni kugonga nyingine karibu na mji wa Sohag, yapata kilomita 500 kusini mwa mji mkuu Cairo.

Taarifa ya idara hiyo imeongeza kuwa, ajali hiyo ilitokea baada ya 'mtu asiyejulikana' kufunga breki ya dharura ya treni moja, ndipo ikagongwa kwa nyuma na nyingine. Magari matatu ya abiria yamehusika pia katika ajali hiyo.

Ripoti zinasema idadi ya watu waliofariki dunia au kujeruhiwa katika ajali hiyo huenda ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi waliopelekwa hospitalini.

Ajali nyingine ya treni iliyotokea Cairo miaka kadhaa nyuma

Usafiri wa garimoshi umekuwa ukikumbwa na ajali mbaya za mara kwa mara nchini Misri ambazo mara nyingi husababisha vifo vya idadi kubwa ya watu.

Wananchi wa Misri wanailaumu serikali ya nchi hiyo kwa kuzembea kuboresha sekta ya usafiri wa garimoshi na kupuuza maisha ya wasafiri.  Mwaka 2017,  watu wasiopungua 36 walifariki dunia baada ya magarimoshi mawili kugongana katika mkoa wa Alexandria nchini Misri.

Tags