UN yaingilia kati mpango wa Kenya wa kufunga kambi kuu za wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i68876-un_yaingilia_kati_mpango_wa_kenya_wa_kufunga_kambi_kuu_za_wakimbizi
Shirika la Kuhudumua Wambizi la Umoja wa Mataifa UNCHR kupitia taarifa iliyotolewa jana mjini Geneva Uswisi, limetangaza kushirikiana na Kenya na kuweka mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kupata suluhisho kwa mgogoro wa wakimbizi wanaoishi katika kambi za Dadaab na Kakuma za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 10, 2021 08:12 UTC
  • UN yaingilia kati mpango wa Kenya wa kufunga kambi kuu za wakimbizi

Shirika la Kuhudumua Wambizi la Umoja wa Mataifa UNCHR kupitia taarifa iliyotolewa jana mjini Geneva Uswisi, limetangaza kushirikiana na Kenya na kuweka mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kupata suluhisho kwa mgogoro wa wakimbizi wanaoishi katika kambi za Dadaab na Kakuma za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Hii ni baada ya serikali ya Kenya kutangaza nia ya kuzifunga kambi hizo za wakimbizi zinazowahifadhi wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi takribani 430,000.

Ili kuelekea katika suluhisho endelevu, UNHCR imesema, kwa kushirikiana na serikali ya Kenya watachukua hatua ikiwemo kuboresha urejeaji wa khiari kwa usalama na hadhi huku wakizingatia vizuizi vya kutembea vinavyohusiana na janga la Covid-19 linaloendelea kuisumbua dunia.  

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Kuweka mipango mbadala ya wakimbizi wanaotoka katika nchi za Afrika Mashariki kuweza kubaki na hii ikimaanisha kuwapa fursa kubwa wakimbizi kuweza kujitegemea na kuchangia katika uchumi wa eneo husika."

UNHCR imesema, kuongeza kasi ya kutolewa kwa vitambulisho vya kitaifa kwa zaidi ya Wakenya 11,000 ambao hapo awali walitambuliwa kama waliosajiliwa katika hifadhi ya data za wakimbizi, na kuendelea kwa mchakato wa uhakiki kwa wengine walioko katika hali kama hizo na pia kuhamishiwa katika nchi za tatu wakimbizi wachache ambao hawawezi kurudi katika nchi zao na wanakabiliwa  na hatari za ulinzi. 

Maafisa usalama wakilinda doria katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab

Fathiaa Abdalla, Mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya amesema, "Tumesikia wasiwasi uliooneshwa na Serikali ya Kenya na tunatumaini kuwa hatua hizi zitakuwa hatua muhimu katika kuharakisha suluhisho endelevu kwa wale wote wanaohusika."  

Aidha afisa huyo wa UNHCR amesema, “tunaamini kwamba kupitia hatua mpya za pamoja tunaweza kuweka hatua zinazoheshimu haki za wakimbizi na kusababisha suluhisho endelevu. Tunatarajia kuendelea na mazungumzo na ushirikiano wetu na mamlaka na washirika wa Kenya juu ya jambo hili muhimu."