Ujumbe wa Sudan kufanya safari rasmi ya kuelekea Israel wiki ijayo
(last modified Thu, 15 Apr 2021 12:51:20 GMT )
Apr 15, 2021 12:51 UTC
  • Ujumbe wa Sudan kufanya safari rasmi ya kuelekea Israel wiki ijayo

Maafisa wawili wa Sudan wamefichua kuwa, ujumbe wa serikali ya nchi hiyo utafanya ziara ya kwanza rasmi kuelekea Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu) wiki ijayo.

Mmoja wa maafisa hao ambaye hakutaka jina lake litajwe amevieleza vyombo vya habari kwamba, maafisa kadhaa wa usalama na intelijensia watakuwemo kwenye ujumbe huo wa serikali ya Khartoum utakaoelekea Tel Aviv.

Kwa mujibu wa maafisa hao, safari hiyo inafanyika kwa lengo la kuimarisha uhusiano baina ya Sudan na utawala haramu wa Israel.

Maafisa rasmi wa pande hizo mbili hawajatoa tamko lolote kuthibitisha au kukadhibisha habari hiyo.

Kufuatia hatua ya serikali ya Sudan ya kufuta sheria inayopiga marufuku kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Jumamosi iliyopita, ujumbe wa serikali ya Sudan ulikutana na ujumbe wa Kizayuni katika nchi ya tatu ya Kiarabu na kufanya mazungumzo kuhusu mashirikiano ya pande mbili hususan katika nyanja za kiuchumi.

Wasudan wakiandamana kuunga mkono Palestina na kupinga kuanzisha uhusiano na Israel

Mwishoni mwa mwaka uliopita, na kwa upatanishi wa Marekani, Sudan na utawala haramu wa Israel zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia.

Hatua hiyo ilipingwa na kulalamikiwa vikali na wananchi na vyama vya siasa nchini Sudan, lakini watawala wa Khartoum hawakujali malalamiko hayo na wakaamua kuendeleza mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina ukiwemo mji wa Baitul Muqaddas, kilipo kibla cha kwanza cha Waislamu…/

 

Tags