Watekaji nyara watishia kuua makumi ya wanafunzi wa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69194-watekaji_nyara_watishia_kuua_makumi_ya_wanafunzi_wa_nigeria
Genge la wabeba silaha lililoteka wanafunzi karibu 30 wa taasisi moja ya elimu ya juu katika jimbo la Kaduna huko kaskazini magharibi mwa Nigeria mwezi uliopita limetishia kuwaua vijana hao wa kike na kiume, baada ya serikali kukataa kuwapa kikomboleo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 18, 2021 22:23 UTC
  • Watekaji nyara watishia kuua makumi ya wanafunzi wa Nigeria

Genge la wabeba silaha lililoteka wanafunzi karibu 30 wa taasisi moja ya elimu ya juu katika jimbo la Kaduna huko kaskazini magharibi mwa Nigeria mwezi uliopita limetishia kuwaua vijana hao wa kike na kiume, baada ya serikali kukataa kuwapa kikomboleo.

Watekaji nyara hao wanataka kupewa kikomboleo cha Naira milioni 300 ili wawaachie huru wanafunzi 29 wa chuo cha Federal College of Forestry Mechanisation, Afaka, kaskazini mwa jimbo la Kaduna.

Gavana wa Kaduna, Nasir El-rufai amekataa katakata ombi la wazazi wanaotaka afanye mazungumzo na watekaji hao, ili kujadili masuala ya kikomboleo. 

Friday Sanni, mwakilishi wa wazazi wa wanafunzi waliotekwa amesema wamekuwa wakipigiwa simu na watekaji hao, ambao wanatishia kuwa watawaua wanafunzi wa kiume na kuoa kwa nguvu wanafunzi wa kike.

Inaarifiwa kuwa, wanafunzi 10 miongoni mwa waliokuwa wametekwa nyara na majambazi hao wameachia huru, baada ya wazazi wao kukubali kulipa kikomboleo.

Gavana wa Kaduna akiongoza mkutano wa usalama

Jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa limefanikiwa kuwanusuru wanafunzi 180 chuoni hapo baada ya kujiri utekaji nyara huo mnamo Machi 12. Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na tukio hilo la utekaji nyara, ingawaje karibu miezi miwili iliyopita wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram liliwateka nyara zaidi ya wanafunzi wa kiume 300 katika jimbo la Katsina huko Nigeria. 

Matukio ya kutekwa nyara wanafunzi yamekithiri huko Nigeria katika miezi ya hivi karibuni, baadhi wakitekwa na magenge ya kigaidi, huku wengine wakitekwa na makundi ya wabeba silaha ambayo huitisha vikomboleo vikubwa.