Polisi ya Nigeria yaua 'majambazi' 30 kaskazini magharibi mwa nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69276-polisi_ya_nigeria_yaua_'majambazi'_30_kaskazini_magharibi_mwa_nchi
Jeshi la Polisi la Nigeria limetangaza kuwa limeua wabeba silaha 30, baada ya genge la majambazi kuvamia vijiji vinne huko kaskazini magharibi mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2021 01:50 UTC
  • Polisi ya Nigeria yaua 'majambazi' 30 kaskazini magharibi mwa nchi

Jeshi la Polisi la Nigeria limetangaza kuwa limeua wabeba silaha 30, baada ya genge la majambazi kuvamia vijiji vinne huko kaskazini magharibi mwa nchi.

Mohammed Shehu, Msemaji wa Polisi katika jimbo la Zamfara la kaskazini magharibi la Nigeria amesema majambazi waliouawa wanashukiwa kuwa wanachama wa magenge ya wabeba silaha yanayoshambulia vijiji na kuteka watu nyara.

Amesema genge hilo la wabeba silaha mapema jana lilivamia vijiji vya Gobirawa, Gora, Rini na Madoti Dankule katika jimbo la Zamfara, lakini lilikabiliwa vikali na maafisa wa polisi katika eneo hilo. Amesema 30 miongoni mwa majambazi hao waliokuwa wamefunikiza nyuso zao wameuawa huku wengine wakitorokea msituni. 

Msemaji wa Polisi ya jimbo la Zamfara ameongoza kuwa, magenge hayo ya wabeba silaha yameshadidisha vitendo vya utekaji katika miezi ya hivi karibuni, huku yakiitisha vikomboleo vikubwa. 

Genge la wabeba silaha jimboni Zamfara

Haya yanajiri siku chache baada ya genge la wabeba silaha lililoteka wanafunzi karibu 30 wa taasisi moja ya elimu ya juu katika jimbo la Kaduna huko kaskazini magharibi mwa Nigeria mwezi uliopita, kutishia kuwaua vijana hao wa kike na kiume, baada ya serikali kukataa kuwapa kikomboleo.

Matukio ya kutekwa nyara watu hususan wanafunzi yamekithiri huko Nigeria katika miezi ya hivi karibuni, baadhi wakitekwa na magenge ya kigaidi, huku wengine wakitekwa na makundi ya wabeba silaha ambayo huitisha vikomboleo vikubwa.