Serikali ya Nigeria yaufungia mtandao wa Twitter kwa muda usiojulikana
Serikali ya Nigeria imetangaza kuwa, hatua ya mtandao wa kijamii wa Twitter ya kuufuta ujumbe mmoja wa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo haikubaliki kabisa hivyo Abuja ameamua kuufungia mtandao huo kwa muda usiojulikana. Twitter kwa upande wake imesema inafuatilia kwa kina suala hilo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, jana Jumatano, mtandao wa Twitter ulitangaza kuwa umeufuta ujumbe wa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria kutokana na ujumbe huo kutoa vitisho kwa watu ambao wanadhaniwa walihusika kushambulia majengo ya serikali. Twitter imedai kuwa ujumbe huo umekwenda kinyume na sera na siasa za mtandao huo.
Hesabu ya Twitter ya Rais Buhari ilifungiwa kwa muda wa masaa 12 na mtandao huo wa kijamii.
Hata hivyo vyombo vya habari vinasema kuwa, licha ya serikali ya Nigeria kutoa tangazo la kuifungia Twitter, lakini mtandao huo wa kijamii hadi wakati tunaandaa habari hii ulikuwa unaendelea kufanya kazi kama kawaida ndani ya Nigeria.
Katika tamko lake, serikali ya Nigeria haikusema amri ya kuufungia mtandao wa kijamii wa Twitter itaanza kutekelezwa lini na saa ngapi. Tangazo limesema tu kuwa Serikali ya Nageria imeifungia Twitter kwa muda usiojulikana.
Kama tulivosema, kwa upande wake, Twitter imesema inafuatilia kwa karibu uamuzi huo wa serikali ya Nigeria.