Jumuiya za kimataifa zalaani hatua ya Nigeria ya kuifungia Twitter
-
Muhammadu Buhari
Jumuiya za kimataifa na balozi za nchi za kigeni nchini Nigeria zimelaani hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuufungia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa muda usiojuliikana.
Shirika kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani hatua hiyo ya serikali ya Abuja likisisitiza kuwa mtandao huo ni ukumbi wa mawasiliano ya kijamii unaotumiwa sana na Wanigeria kwa ajili ya kutekeleza haki zao za kibinadamu ikiwemo haki ya kusema na kujieleza.
Umoja wa Ulaya, Uingereza na Canada pia zimelaani hatua hiyo ya serikali ya Nigeria zikisema kuwa zimevunjwa moyo na hatua hiyo.
Serikali ya Abuja imeamua kuufungia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa muda usiojulikana baada ya mtandao huo kufuta ujumbe mmoja wa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo.
Siku ya Jumamosi, Waziri wa Sheria wa Nigeria alisema Wanigeria wanaojaribu kukiuka marufuku ya serikali dhidi ya Twitter watafunguliwa mashtaka.
Jumatano iliyopiita mtandao wa Twitter ulitangaza kuwa umeufuta ujumbe wa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria kutokana na ujumbe huo kutoa vitisho kwa watu ambao wanadhaniwa walihusika kushambulia majengo ya serikali. Twitter imedai kuwa ujumbe huo umekwenda kinyume na sera na siasa za mtandao huo.