Eritrea yailaumu Marekani kwa kuchochea mapigano Tigray, Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71032-eritrea_yailaumu_marekani_kwa_kuchochea_mapigano_tigray_ethiopia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea amezilaumu tawala za Marekani kwa kuchochea mapigano na vita katika eneo la Tigray, la kaskazini mwa Ethiopia kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 08, 2021 03:42 UTC
  • Eritrea yailaumu Marekani kwa kuchochea mapigano Tigray, Ethiopia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea amezilaumu tawala za Marekani kwa kuchochea mapigano na vita katika eneo la Tigray, la kaskazini mwa Ethiopia kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Katika barua yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Osman Saleh, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Eritrea amesema kitendo cha serikali ya sasa na zilizopita za Marekani kuwaunga mkono viongozi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) kwa muda miaka 20 ndilo chimbuko la mapigano ya hivi sasa katika eneo hilo.

Amesema kitendo cha Washington cha kuilaumu Eritrea kwa mapigano hayo ya Tigray hakina msingi wowote. Waziri huyo wa Eritrea ameukashifu utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani kwa kushadidisha mgogoro na ukosefu wa uthabiti kwa kuingilia masuala ya ndani ya eneo hilo la Pembe ya Afrika.

Ethiopia ilitangaza hivi karibuni kuwa wanajeshi wa nchi jirani ya Eritrea wanaotuhumiwa kuua mamia ya raia wa Ethiopia wameanza kuondoka katika eneo linalokumbwa na mgogoro la Tigray lililo katika mpaka baina ya nchi hizo mbili za Afrika.

Mapigano katika eneo la Tigray

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana, kwa madai kuwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wameuawa na wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo ya eneo la Tigray.