Burkina Faso yaahidi kuwafyekelea mbali wahusika wa mashambulizi ya karibuni
Christophe Dabire Waziri Mkuu wa Burkina Faso ameahidi kuwa shambulizi lililofanywa hivi karibuni katika kijiji cha Solhan na wanamgambo wenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo na kuuwa watu 160 halitanyamaziwa kimya. Amesema shambulio hilo la kinyama halitapita hivihivi bila ya kuchukuliwa hatua wale wote waliohusika na jinai hiyo.
Waziri Mkuu wa Burkina Faso ameeleza hayo alipokutana na raia wakazi wa kijiji cha Solhan ambao hivi sasa wamepata hifadhi katika eneo la Sebba makao makuu ya jimbo la Yagha. Ameongeza kuwa, serikali inatumai kuwa itaweza kujipanga na kuhudumia raia hao waliokimbia makazi yao kufuatia shambulio la wanamgambo wenye silaha.
Amesema usalama umeimarishwa katika eneo palipojiri shambulio hilo na msako mkali unaendelea wa kuwasaka wahalifu.
Itakumbukwa kuwa, usiku wa Ijumaa iliyopita watu waliokuwa na silaha walikishambulia kijiji cha Solhan katika jimbo la Yagha huko katika eneo la Sahel na kuuwa watu 132 kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Burki Faso. Wakati huo huo duru za ndani zinasema kuwa watu 160 waliuawa katika hujuma hiyo.
Burkina Faso nchi inayopatikana katika eneo la Sahel barani Afrika imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya wanamgambo wenye misimamo mikali kwa muda wa miaka sita sasa.