Waafrika milioni 146 wanakufa kila mwaka kwa magonjwa yanayohusishwa na tumbaku
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71424-waafrika_milioni_146_wanakufa_kila_mwaka_kwa_magonjwa_yanayohusishwa_na_tumbaku
Shirika la Afya Duniani (WHO) limefichua kuwa, watu wasiopungua milioni 146 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yanayonasibishwa na matumizi ya tumbaku barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 19, 2021 00:42 UTC
  • Waafrika milioni 146 wanakufa kila mwaka kwa magonjwa yanayohusishwa na tumbaku

Shirika la Afya Duniani (WHO) limefichua kuwa, watu wasiopungua milioni 146 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yanayonasibishwa na matumizi ya tumbaku barani Afrika.

Dakta Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa Kieneo wa Shirika la Afya Duniani barani Afrika amesema kuwa, mbali na uvutaji sigara, lakini matumizi ya bidhaa za tumbaku kama vile uvutaji wa mvuke wa tumbaku kwa kutumia kifaa maalumu (vaporizer) yameongezeka kwa kiwango cha kutisha barani humo.

Moeti amesema watu zaidi ya milioni moja na laki mbili wanaaga dunia kila mwaka kote duniani kutokana na athari ya moshi wa wavuta sigara, wakiwemo makumi ya maelfu watoto wadogo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, zaidi ya watu milioni nane wanafariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku kote duniani. Kwa mujibu wa takwimu za WHO, kuna wavutaji sigara zaidi ya bilioni 1.1 duniani kote.

Bidhaa za tumbaku

Mkurugenzi wa Kieneo wa WHO barani Afrika ameeleza bayana kuwa, matumizi ya tumbaku mbali na kusababisha maafa, yanaongeza pia viwango vya umasikini, kupunguza ukuaji wa uchumi, kuvunjika kwa ndoa, mbali na kuchafua mazingira. 

Dakta Moeti ameongeza kuwa, ni jambo la kusikitisha kuona matumizi ya tumbaku yanasalia kuwa sababu kuu ya vifo vinavyoweza kuzuilika duniani. Amesema, "kuacha uraibu wa tumbaku ni muhali, lakini leo ni siku nzuri ya kuanza."