Sudan katika lindi la maandamano mapya ya wananchi
Mgogoro wa kisiasa na kuchumi unaendele kuisumbua Sudan licha ya kupita miaka miwili sasa tangu baada ya harakati ya wananchi iliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa miaka 30 wa Omar al Bashir na kuundwa serikali mpya nchini humo.
Wasudani wamemiminika tena mitaani wakipinga siasa za serikali ya nchi hiyo na sera zake za kiuchumi wakitaka kuondoka madarakani serikali ya Khartoum kwa madai kwamba, imeshindwa kutimzia matarajio ya Wasudani.
Omar al Bashir aliyekuwa rais wa Sudan aliondolewa madarakani mwezi Aprili mwaka 2019 baada ya machafuko makubwa na maandamano ya wananchi yaliyochochea mapinduzi ya jeshi. Wakati huo Wasudani walilalamikia hali mbaya ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, umaskini mkubwa, vita na machafuko ya ndani na maamuzi yasiyofaa ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kujiunga nchi hiyo katika muungano vamizi dhidi ya taifa la Yemen.
Baada ya kuondolewa madarakani Omar al Bashir, baraza la kijeshi lililoongozwa na Abdul Fattah al Burhan lilichukua madaraka ya nchi hiyo na baadaye kuliundwa serikali ya mpito baada ya mauaji ya mamia ya waandamanaji. Serikali hiyo iliahidi kuboresha hali ya kiuchumi na kisiasa, kuzingatia matakwa ya wananchi na kutayarisha mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki. Hata hivyo hivi sasa baada ya kupita miaka miwili tangu serikali ya mpito ishike madaraka ya nchi, Sudan inaendelea kuandamwa na migogoro mingi hususan katika upande wa masuala ya kiuchumi na hali mbaya ya kimaisha. Ukosefu wa ajira, umaskini na hali mbaya ya kiuchumi vimewafanya Wasudani wengi wakose matumaini ya serikali ya sasa ya nchi hiyo. Uamuzi wa serikali ya Khartoum wa kufuta ruzuku ya mafuta na dizeli umepelekea kuongeza mfumuko wa bei kwa zaidi ya asilimia 360 nchini humo. Kwa kuzingatia hali hiyo, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Sudan limetangaza kuwa: Kuongezwa bei ya nishati kunaonesha kuwa, serikali ya mpito haiwajali wananchi na matakwa yao.
Katika kipindi cha mika miwili iliyopita serikali ya Khartoum ilisalimu amri mbeye ya siasa na matakwa ya Washington ikiwa ni pamoja na kukubali kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia ya utawala wa Kizayuni wa Israel na hata kuendelea kuwepo katika muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya taifa la Yemen licha ya upinzani mkali wa wananchi, ili asaa ikapata himaya ya misaada ya Washington na Riyadh katika kutatua matatizo ya kiuchumi. Hata hivyo kujisalimisha huko kwa matakwa ya Washington hakukuisaidia lolote serikali ya Sudan, bali kumezidisha hasira za wananchi. Chama cha Kikomunisti cha Sudan kimetoa taarifa kikitangaza masikitiko yake kutokana na uamauzi wa serikali ya Khartoum wa kuanzisha uhusiano na dola haramu la Israel na kimeikosoa Marekani kwa kutotekeza ahadi yake ya kuwekeza katika miradi ya kilimo na teknolojia nchini Sudan.
Baada ya kushika hatamu serikali ya mpito nchini Sudan ilitarajiwa kuwa nchi hiyo itashuhudia siku na hali bora zaidi katika siku za usoni. Hata hivyo matarajio hayo yalikuwa sawa na mazigazi tu, na mpaka sasa serikali ya Khartoum haijaweza kuboresha hali ya nchi hiyo. Mdororo wa uchumi na hali mbaya ya kisiasa vinaendelea kuizonga Sudan, na wananchi wanatumbukia katika umaskini na hali mbaya ya maisha siku baada ya nyingine. Hali imekuwa mbaya nchini Sudan kiasi kwamba, sasa vyama vya upinzani vinapanga kuitisha maandamano ya kuiondoa madarakani serikali ya Khartoum. Katibu Mkuu wa chama cha Kongresi ya Taifa, Bashir Adam Rahma anasema: Zinafanyika jitihada za kuiondoa madarakani serikali ya sasa na kuunda serikali mpya itakayojumuisha makundi na matabaka yote ya wananchi.
Ripoti kutoka Sudan zinasema kumeshuhudia mapigano makali baina ya waandamanaji na askari usalama katika maeneo mbalimbali ya Sudan na kwamba polisi wametumia gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya wanchi. Serikali inawatuhumu waandamanji kuwa wamemiminika mitaani kutii matakwa ya mabaki ya viongozi wa zamani wa nchi hiyo.
Waandamanaji hao wanataka kuondolewa madarakani viongozi wa serikali na jeshi la Sudan kwa hoja kuwa, wameshindwa kutimiza matakwa ya mapinduzi yaliyoiondoa madarakani serikali ya dikteta wa zamani, Omar al Bashir. Wanaharakati wa Sudan wameapa kuwa, wataendeleza maandamano hadi pale matakwa ya wananchi yatakapotekelezwa
Kwa kutilia maanani hali hiyo inaonekana kuwa, Sudan inakabiwa na kiangazi chenye joto kali sana la kisiasa.