Kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky yapigwa tarehe tena nchini Nigeria
Mahakama ya Nigeria imeipiga tena tarehe kesi ya kiongozi wa Harakati ya Kisilamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Julai.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa jimbo la Kaduna huko Nigeria ametangaza kuwa, sababu za kuakhirishwa tena kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni kutofikia maamuzi kuhusu kesi hiyo na kutotumwa mahakamani hapo faili la kesi hiyo baada ya kufanyika kikao cha maneno cha kusikiliza kesi hiyo.
Mshauri wa kisheria wa Sheikh Zakzaky amekabidhi faili la kesi baada ya maamuzi ya mahakama na kuitaka timu ya mahakama ya Kaduna katika shauri hilo ichukue maamuzi yanayotakiwa.
Sheikh Ibrahim Zakzaky alikamatwa na wanajeshi wa Nigeria tarehe 13 Disemba 2015 pamoja na mkewe baada ya wanajeshi wa serikali kushambulia eneo lake la mikutano huko Zaria.
Uvamizi huo wa wanajeshi wa Nigeria uliua mamia ya watu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Ibrahim Zakzaky. Wanajeshi wa Nigeria walimpiga risasi kadhaa kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kabla ya kumkamata.
Mahakama Kuu ya Nigeria imetoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini serikali inakataa kutekeleza amri ya mahakama.
Hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky imezidi kuwa mbaya katika miezi ya hivi karibuni. Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu, mara kwa mara yamekuwa yakiitaka serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria iheshimu amri ya Mahakama Kuu na imuachilie huru kiongozi huo wa kidini.
Katika miezi ya hivi karibuni, wananchi wa Nigeria wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara ya kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe.