Indhari kuhusu hatari ya kujiri vita vya ndani huko Sudan
Chama kimoja cha kisiasa nchini Sudan kimetahadharisha kuhusu mapigano yanayoendelea kati ya makundi ya wanamgambo na kuwepo hatari ya kujiri vita vya ndani nchini humo.
Chama cha Umoja wa Shirikisho cha nchini Sudan kimeashiria namana kamanda wa kikosi cha radiamali ya haraka nchini humo anavyopinga kujumuishwa jeshini vikosi vya chama hicho na kutangaza kuwa, mapigano yoyote kati ya askari jeshi yatapelekea kuibuka mapigano ya ndani huko Sudan. Kwa hiyo ni vyema askari jeshi wakaweka pembeni hitilafu zao.
Chama cha Umoja wa Shirikisho kimesisitiza pia kwamba kinataka kufanyika mageuzi katika idara za usalama na vikosi vya jeshi huko Sudan na kwamba chama hicho kinaunga mkono kujumuishwa jeshini makundi yote ya wanamgambo yanayobeba silaha. Maandamano ya wananchi dhidi ya serikali ya aliyekuwa mtawala wa nchi hiyo Omar al Bashir yalianza nchini humo tangu mwezi Disemba mwaka 2018; na mwezi Aprili mwaka 2019 al bashir aluzuliwa madarakani na sasa Sudan inaongozwa na serikali ya mpito.
Katika miezi ya karibuni Sudan imekumbwa na mivutano ya kisiasa na mapigano ya silaha katika maeneo kadhaa nchini humo; khususan katika maeneo ya jimbo la Darfur, mashariki mwa Sudan na huko Kordofan Kusini.