Aug 02, 2021 06:56 UTC
  • Wanajeshi 15 wa Niger wauawa katika shambulio la kigaidi huko Torodi

Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza kuwa, kwa akali wanajeshi wake 15 wameuawa kufuatia shambulio la kigaidi kusini magharibi mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger imeeleza pia kuwa, wanajeshi 7 wa serikali ya nchi hiyo wamejeruhiwa vibaya pia huku wanajeshi wengine 6 hawajulikani walipo.

Shambulio hilo la kigaidi limetokea katika eneo la Torodi kusini magharibi mwa Niger katika mpaka wa nchi hiyo na Burkina Faso, imeeleza taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger imeeleza kuwa, jeshi la nchi kavu likisaidiwa na ndege za kivita limo katika kutekeleza operesheni kubwa kwa ajili ya kuangamiza magaidi  katika maeneo hayo ya kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Wanajeshi wa Niger wakiwa katika  operesheni ya kuwasaka magaidi

 

Eneo la Torodi lipo kusini mashariki mwa mji wa Tillaberi uunaopakkana na Burkina Faso na Mali.

Bado haijajulikana ni kundi au makundi yepi yaliyohusika na hujuma hiyo, lakini eneo hilo linadhibitiwa na vikundi vyenye uhusiano na magenge ya al Qaeda na Daesh.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, raia 19 waliuawa hivi karibuni kwenye shambulizi linaloaminika kuwa la kigaidi katika mpaka wa Niger na Mali.

Maeneo mbali mbali ya Niger yamekuwa yakiandamwa na mashambulio ya mara kwa mara ya umwagaji damu ya makundi ya wabeba silaha yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS).

Tags