Sudan yasema Bwawa la an-Nahdha linahatarisha viwanda vyake vya kuzalisha umeme
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amedai kwamba serikali ya nchi hiyo kutokuwa na habari kuhusu mwenendo wa kujazwa maji Bwawa la an-Nahdha katika nchi jirani ya Ethiopia ni tishio kwa viwanda vyake vya kuzalisha umeme.
Madai hayo yametolewa na Mariam al-Sadiq al-Mahdi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan ambaye ameongeza kwamba nchi yake inakaribisha pendekezo lililotolewa na Algeria la kuwataka viongozi wa nchi tatu za Misri, Ethiopia na Sudan waketi kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya kutafuta njia ya kutatua hitilafu zilizopo kuhusu ujenzi wa Bwawa la an-Nahdha.
Tayari Algeria imeanzisha juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kusaidia kutatua tofauti hizo. Ramtane Lamamra, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria ambaye ameteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa Rais Abdelmadjid Tebboune wa nchi hiyo katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa bwawa hilo tayari amewasilisha mpango wa utatuzi wa mgogo huo kwa viongozi wa nchi tatu hizo.
Ujenzi wa Bwawa la an-Nahdha katika vyanzo vya Mto Nile nchini Ethiopia, umekuwa chanzo cha ugomvi mkubwa wa maji kati ya nchi hiyo na Sudan na vile vile Misri tangu mwaka 2011.
Kwa mujibu wa Misri, kujazwa Bwawa la An-Nahdha na maji ya Mto Nile kunaweza kuibua mgogoro mkubwa wa maji katika nchi hiyo na jirani yake Sudan, mgogoro ambao unaweza pia kuvikumba vizazi vijavyo vya nchi mbili.
Mazungumzo ya nchi tatu hizo kuhusu bwawa hilo na ambayo yanasimamiwa na Umoja wa Afrika hayajakuwa na matunda yoyote ya kuridhisha hadi sasa.