Walioteka nyara makumi ya watoto nchini Nigeria wataka kikomboleo
Watu wenye silaha waliowateka nyara takribani watoto 80 katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria, wametaka walipwe fedha za kuwakombolea mateka hao.
Kasisi mmoja ambaye amefanya mazungumzo na watekaji nyara hao amesema kuwa, watu hao wenye silaha wanataka dola 2400 kwa kila mwanafunzi ambapo hadi sasa wanawashikilia mateka wanafunzi wasiopungua 80.
Katikati ya mwezi uliopita, kundi moja la wanamgambo wenye silaha liliwateka nyara wanafunzi 108 katika shambulio lililofanya katika shule moja ya sekondari katika jimbo la Kaduna, huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Baada ya siku mbili, watekaji nyara hao waliwaachia huru wanafunzi 28, na hadi sasa wameendelea kuwashikilia mateka wanafunzi 80 na kueleza kwamba, hawako tayari kuwaachilia huru watoto hao wa shule hadi watakapolipwa kikomboleo.
Jimbo la Kaduna huko kaskazini magharibi mwa Nigeria limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha na kesi za kutekwa nyaraka mamia ya wanafunzi kila mara limegeuka na kuwa jambo la kawaida kabisa katika jimbo hilo.
Mwaka 2014 pia zaidi ya wanafunzi 270 wa kike walitekwa nyara na genge la kigaidi la Boko Haram mjini Chibok Nigeria.
Serikali ya Nigeria inayoongozwa na Rais Muhamadu Buhari inaandamwa na ukosoaji mkali kieneo na kimataifa kutokana na kushindwa kukabiliana na changmoto za usalama zinazoikabili nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.