Maelfu ya watu waandamana Ghana dhidi ya serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73152-maelfu_ya_watu_waandamana_ghana_dhidi_ya_serikali
Maelfu ya watu wamejitokeza mabarabarani katika mji mkuu wa Ghana, Accra kushiriki maandamano dhidi ya serikali ya Rais Nana Akufo-Addo wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2021 22:02 UTC
  • Maelfu ya watu waandamana Ghana dhidi ya serikali

Maelfu ya watu wamejitokeza mabarabarani katika mji mkuu wa Ghana, Accra kushiriki maandamano dhidi ya serikali ya Rais Nana Akufo-Addo wa nchi hiyo.

Katika maandamano hayo ya jana Jumatano, waandamanaji hao waliokuwa wamevalia mavazi mekundu na meusi walisikikia wakipiga nara dhidi ya utawala wa Akufo-Addo.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na jumbe zinazosema: Tengeneza nchi yetu, Ufisadi unazalisha umaskini; rekebisha mfumo wa elimu na kadhalika.

Mmoja wa waandamanaji hao, Frederick Koomson (28), muuzaji wa simu za rununu amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, "Nana Akufo-Addo, tunahangaika, tufanyie jambo, mambo yameharibika, serikali inapaswa kuamka."

Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana

Nana Akufo-Addo alichaguliwa kwa muhula wa pili kuwa Rais wa Ghana katika uchaguzi wa Disemba mwaka jana 2010, kwa kupata asilimia 51.59 ya kura zilizopigwa.

Maandamano ya jana ni kati ya maandamano makubwa ambayo yameshuhudiwa nchini humo tokea Machi mwaka huu, baada ya mahakama kutupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, iliyowasilishwa na mpinzani mkuu wa Akufo-Addo katika uchaguzi huo, John Mahama, aliyeambulia asilimia 47.36 ya kura.