UN: Watu laki mbili wamekuwa wakimbizi kutokana na vita nchini Ethiopia
Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa, watu laki mbili wamekuwa wakimbizi katika jimbo la Amhara na wengine elfu 45 katika jimbo la Afar huko Ethiopia kutokana na mapigano nchini humo.
Martin Griffith Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia amewaambia waandishi wa habari kuwa, watu laki mbili wamekuwa wakimbizi huko Amharana elfu 45 huko Afar kufuatia mapigano yanayoendelea huko Tigray na kwamba malori 100 yanahitajika kwa siku ili kufikisha misaada ya kibinadamu huko Tigray.
Mapigano kati ya serikali ya Ethiopia na waasi wenye mfungamano na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) yalianza mwezi Novemba mwaka janakatika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Mapigano hayo hadi sasa yamesababisha watu milioni mbili kuyahama makazi yao na wengine laki nne kukabiliwa na ukosefu wa chakula.