'Magaidi' 78 wauawa katika mashambulio ya anga ya jeshi la Nigeria
Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuua makumi ya wahalifu wanaobeba silaha katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa nchi.
Msemaji wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Nigeria, Edward Gabkwet amesema wabeba silaha wapatao 78 waliuawa katika operesheni iliyofanywa hivi karibuni na askari wa nchi hiyo, yakiwemo mashambulio ya anga.
Gabkwet amesema majambazi hao waliokuwa juu ya pikipiki, waliuawa Agosti 2 wakielekea katika Msitu wa Kwiambana jimboni Zamfara.
Msemaji huyo wa Jeshi la Nigeria amebainisha kuwa, jeshi la nchi hiyo ya Afrika Magharibi lilitumia ndege za kivita za Alpha pamoja na helikopta kushambulia kwa mabomu maficho ya wabeba silaha hao.
Magenge ya wabeba silaha yamekuwa yakifanya mashambulizi na mauaji ya kutisha katika jimbo la Zamfara, eneo ambalo kwa kipindi kirefu sasa limekuwa likishuhudia umwagaji damu na mapigano.
Jimbo hilo la Kaskazini Magharibi mwa Nigeria limeshuhudia pia ongezeko la visa vya kutekwa nyara wanafunzi vinavyofanywa na magenge ya uhalifu yanayobeba silaha, ambayo huishia kuitisha vikombolea vikubwa.