Sudan kumkabidhi al Bashir kwa mahakama ya ICC
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amesema kuwa, viongozi wa nchi hiyo wamechukua uamuzi wa kumkabidhi rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir na makamu wake wawili kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) huko Hague nchini Uholanzi.
Katika mazungumzo yake na Karim Khan Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama ya ICC mjini Khartoum, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Mariam Sadiq al Mahdi amesisitiza kuwa, serikali imeamua kuwakabidhi kwa ICC watu wote waliokuwa wakisakwa na mahakama hiyo. Mariam Sadiq al Mahdi ameongeza kuwa, serikali ya Khartoum imepasisha muswada wa sheria ya Sudan kuijiunge na Mkataba wa Roma uliobuni mahakama ya ICC na kwamba suala hilo linatazamiwa kuidhiishwa katika kikao cha pamoja cha Baraza la Utawala na Serikali.
Kwa upande wake Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ameeleza hamu yake ya kushirikiana na Sudan ili kupatikana uadilifu.
Mwaka 2009 na 2010 mahakama ya ICC ilimtuhumu al Bashir kwamba ametenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika eneo la Darfur magharibi mwa Sudan. Hata hivyo rais huyo wa zamani wa Sudan alikanusha tuhuma hizo na kuitaja mahakama ya ICC kuwa ni ya kisiasa.
Omar al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi la Sudan Aprili 11 mwaka 2019 kufuatia maandamano mtawalia ya wananchi waliokuwa wakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.