Watu 1,500 wakimbia machafuko Darfur, Sudan
Kamisheni Kuu ya Misaada ya Kibinadamu ya Sudan imetangaza kuwa, wakazi elfu moja na mia tano wa Darfur wamelazimika kukimbilia katika kambi za wakimbizi zilioko kaskazini mwa eneo hilo la magharibi mwa Sudan kutokana na ghasia na machafuko yanaoendelea katika eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa mapema leo Alkhamisi na kamisheni hiyo imesema kuwa, machafuko yanayoendelea huko Darfur yamewalazimisha watu elfu moja na mia tano kukimbia makazi yao na kuelekea kwenye kambi za wakimbizi.
Ripoti zinasema, katika siku chache za karibuni vijiji 38 vya Darfur vimekumbwa na mapigano makali ya kugombania ardhi ya kilimo. Ripoti hiyo inasema kuwa, hadi sasa makumi ya watu wameuwa huko Darfur kutokana na mizozo ya kugombania ardhi na ya kikabila.
Mwezi Aprili mwaka huu watu wasiopungua 132 waliouawa katika machafuko ya kikabila yaliyozuka katika mji wa el-Geneina, makao makuu ya Jimbo la Daruf Magharibi nchini Sudan.
Mwaka 2003 eneo la Darfur lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa rais aliyeenguliwa madarakani, Omar al-Bashir, na wapinzani wa serikali. Karibu wakazi 300,000 wa jimbo hilo waliuawa katika mapigano hayo.