Wanamgambo 17 wauawa kaskazini mwa Burkina Faso
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73480-wanamgambo_17_wauawa_kaskazini_mwa_burkina_faso
Wanamgambo 17 wameuawa baada ya kukabiliwa vikali na walinda usalama wa kujitolea huko kaskazini mwa Burkina Faso.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 13, 2021 19:30 UTC
  • Wanamgambo 17 wauawa kaskazini mwa Burkina Faso

Wanamgambo 17 wameuawa baada ya kukabiliwa vikali na walinda usalama wa kujitolea huko kaskazini mwa Burkina Faso.

Gazeti la LeFaso liliripoti hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, wanagambo hao waliokuwa wamejizatiti kwa silaha waliuawa mapema wiki hii katika makabiliano baina yao na askari wa kujitolea katika eneo la Bilakoka lililoko katika eneo Sahel, mpakani mwa nchi hiyo na Mali na Niger. 

Kwa mujibu wa gazeti hilo la Burkinabe, walinda usalama watano wa kujitolea waliuawa pia katika mapigano hayo. 

Kikosi cha Askari wa Kujitolea kiliundwa na serikali ya Burkina Faso Disemba mwaka 2019, kwa lengo la kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo kupambana na magenge ya waasi na magaidi katika ngazi ya vijiji.

Maafisa usalama wa Burkina Faso wakiwa katika operesheni

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wanajeshi wasiopungua 12 wa serikali ya Burkina Faso kuawa katika shambulizi lililofanywa na makundi ya waasi kaskazini mwa nchi hiyo.

Burkina Faso nchi inayopatikana katika eneo la Sahel barani Afrika imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya wanamgambo wenye misimamo mikali na magaidi wakufurishaji kwa miaka mingi sasa.