Makumi ya wanafunzi waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru
Makumi ya wanafunzi wa Chuo cha Kiislamu waliotekwa nyara huko Nigeria katika jimbo la Niger mnano Mei 30 mwaka huu wameachiliwa huru.
Mwalimu Mkuu wa hauza hiyo ya Kiislamu, Abubakar Alhassan amesema ingawaje hawana idadi kamili ya wanafunzi walioachia huru, lakini hivi sasa hakuna mwanafunzi aliyesalia mikononi mwa watekaji hao. Amesema, "wanafunzi wote hivi sasa wameachiwa huru, tunawapeleka majumbani mwao."
Wasimamizi wa shule hiyo ya kidini wanasema wanafunzi 15 kati ya 136 waliotekwa nyara na genge la wabeba silaha katika mji wa Tegina jimboni Niger walifanikia kutoroka mwezi Juni, lakini sita waliripotiwa kuaga dunia wakiwa mikononi mwa watekaji.
Februari mwaka huu, watu 42 wakiwemo wanafunzi 27 waliotekwa nyara katika shule moja ya sekondari ya serikali katika wilaya ya Kagara katika jimbo hilo hilo la Niger waliachiwa huru.
Visa vya utekaji nyara hususan dhidi ya wanafunzi vimekithiri mno katika miezi ya hivi karibuni nchini Nigeria. Magenge yanayobeba silaha nchini humo yamekuwa yakiitisha fedha nyingi kama kikomboleo cha kuwaachia huru watu yanaowashikilia mateka.
Wiki iliyopita, maafisa wa jimbo la Zamfara walieleza kuwa, watu wenye silaha wasiojulikana walishambulia kijiji cha Rini katika jimbo hilo na kuwatekanyara raia wasiopungua 60. Alisema kuna uwezekano pia raia kadhaa waliuawa katika shabulio hilo.
Serikali ya Nigeria inayoongozwa na Rais Muhamadu Buhari inaandamwa na ukosoaji mkali kieneo na kimataifa kutokana na kushindwa kukabiliana na changmoto za usalama zinazoikabili nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.