Mripuko wa kipindupindu waua watu 63 nchini Nigeria
Makumi ya watu wameripotiwa kuaga dunia kutokana na mripuko wa maradhi ya kipindupindu nchini Nigeria.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC) imesema kwamba, mbali na watu 63 kuaga dunia kwa maradhi hayo katika mripuko mpya ndani ya wiki moja baina Agosti 16 na 22, kesi zinazoshukiwa kuwa za ugonjwa huo zimepindukia ni 3,000.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, tangu mripuko huo mpya uliporitiwa kwa mara ya kwanza tarehe 16 mwezi huu wa Agosti, ugonjwa huo umeshaenea katika majimbo 11 ya nchi hiyo, likiwemo jimbo la Katsina anakotokea Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo. Jimbo hilo linaongoza kwa idadi ya vifo baada ya kurekodi vifo 19, likifuatiwa na Bauchi vifo 16.
Kwa mujibu wa NCDC, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa kesi 58,698 za ugonjwa wa kipindupindu zimenakiliwa vikiwemo jumla ya vifo 2,035.
Ugonjwa wa kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya Vibrio Cholera na huenezwa kwa kunywa maji yasiyo salama. Dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika pamoja na homa.
Miripuko ya maradhi hayo hatarishi huripotiwa nchini Nigeria mara kwa mara, hususan katika misimu ya mvua za masika zinazoambatana na mafuriko.