Burundi yaituhumu tena Rwanda kuwa inaharibu usalama wake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7420-burundi_yaituhumu_tena_rwanda_kuwa_inaharibu_usalama_wake
Kwa mara nyingine tena serikali ya Burundi imeituhumu Rwanda kuwa inafanya njama za kuharibu utulivu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2016 02:36 UTC
  • Burundi yaituhumu tena Rwanda kuwa inaharibu usalama wake

Kwa mara nyingine tena serikali ya Burundi imeituhumu Rwanda kuwa inafanya njama za kuharibu utulivu nchini humo.

Redio ya Kimataifa ya Ufaransa imeinukuu serikali ya Burundi ikisema hayo jana Alkhamisi katika ripoti yake ya kurasa 25 kuhusu kuingilia Rwanda mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Kwa muda sasa Burundi imekuwa ikiituhumu Rwanda kuingilia masuala yake ya ndani, ingawa hata hivyo hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Bujumbura kuandaa ripoti maalumu kuhusiana na madai yake hayo.

Historia ya ripoti hiyo inaanzia mwaka 1959 wakati maelfu ya wakimbizi wa Rwanda walipokimbilia Burundi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakimbizi hao wameleta madhara makubwa kwa Burundi madhara ambayo yameshuhudiwa pia katika machafuko yaliyoanza mwaka jana ndani ya Burundi.

Ripoti hiyo ya serikali ya Bujumbura imeongeza kuwa, serikali ya Rwanda inawashawishi wakimbizi wa Burundi kufanya machafuko ndani ya Burundi kwani mfumo wa kisiasa wa Rwanda unaona kuwa, mchakato wa umoja wa kitaifai nchini Burundi ni tishio kwa Rwanda.

Serikali ya Burundi inaamini kuwa, kuweko watu wa makabila tofauti katika serikali ya nchi hiyo ni mafanikio yanayopasa kupongezwa.

Hata hivyo serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha mara kwa mara tuhuma za kuingilia mambo ya ndani ya Burundi.