Watu milioni 7.87 wameambukizwa corona barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i74298-watu_milioni_7.87_wameambukizwa_corona_barani_afrika
Nchi za Kiafrika zilirekodi maambukizi mapya 25,477 ya COVID-19 katika masaa 24 kufikia Jumamosi na hivyo kuifanya jumla ya watu walioambukizwa ugonjwa huo hadi kufikia sasa barani humo kuwa milioni 7.87.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2021 22:46 UTC
  • Watu milioni  7.87 wameambukizwa corona barani Afrika

Nchi za Kiafrika zilirekodi maambukizi mapya 25,477 ya COVID-19 katika masaa 24 kufikia Jumamosi na hivyo kuifanya jumla ya watu walioambukizwa ugonjwa huo hadi kufikia sasa barani humo kuwa milioni 7.87.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika, watu wasiopungua 601 walipoteza maisha kwa sababu zinazohusiana na COVID-19 katika masaa 24 kufikia siku ya Jumamosi na kusababisha vifo vilivyotokana na ugonjwa huo barani humo kuwa 198,587. Idadi ya waliopona COVID-19 hadi sasa ni zaidi ya milioni saba, imeongeza ripoti hiyo.

Kati ya maeneo matano ya kijiografia katika bara hilo, eneo la Kusini mwa Afrika lina kesi nyingi zaidi za COVID-19 ambazo zimefika milioni 3.7 lilifuatiwa na Kaskazini mwa Afrika ambako maambukizi yamefika milioni 2.4 huku ukanda wa Afrika Mashariki ukiwa na kesi 918,400, Afrika Magharibi 610,100 na Afrika ya Kati 221,500.

Kulingana na taarifa, dozi milioni 137.7 za chanjo zimesambazwa hadi sasa kwa ajili ya matumizi katika bara la Afrika lenye wakazi bilioni 1.3, ambapo dozi milioni 104.2 zimeshatolewa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa nchi 42 kati ya 54 za Afrika hazitaweza kuwachanja watu walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa corona. WHO imesema uhaba wa chanjo barani Afrika unatokana na nchi tajiri kuendelea kuhodhi chanjo ya virusi vya corona.