Sisitizo la Umoja wa Afrika la kutuma askari wa kimataifa nchini Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7489-sisitizo_la_umoja_wa_afrika_la_kutuma_askari_wa_kimataifa_nchini_burundi
Umoja wa Afrika AU umetoa ripoti maalumu kuhusiana na uvunjaji wa haki za binadamu nchini Burundi na kusisitizia nia ya umoja huo ya kutuma askari wa kimataifa wa kulinda amani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2016 08:42 UTC
  • Sisitizo la Umoja wa Afrika la kutuma askari wa kimataifa nchini Burundi

Umoja wa Afrika AU umetoa ripoti maalumu kuhusiana na uvunjaji wa haki za binadamu nchini Burundi na kusisitizia nia ya umoja huo ya kutuma askari wa kimataifa wa kulinda amani nchini humo.

Makao Makuu ya AU ya mjini Addis Ababa Ethiopia yamesema katika taarifa yake kwamba, idadi ya askari wa kulinda amani na maafisa wa haki za binadamu wa umoja huo nchini Burundi itaongezwa na kwamba umoja huo utatuma polisi wa kimataifa kwa ajili ya kusimamia amani licha ya wapinzani wa serikali ya Bujumbura kulalamikia suala hilo wakisema kuwa, wanalotaka wao ni kutumwa wanajeshi wa kulinda amani nchini Burundi na sio polisi. Ripoti ya kurasa 58 ya wataalamu wa Umoja wa Afrika imetolewa baada ya kufanyika uchunguzi mwezi Disemba mwaka 2015. Mgogoro wa nchini Burundi ulianza mwezi Aprili mwaka jana wakati Rais Pierre Nkurunzinza alipoidhinishwa na chama chake cha CNDD-FDD kugombea urais kwa mara ya tatu mfululizo. Vyama vya upinzani na asasi za kiraia ziliitisha maandamano makubwa hasa jijini Bujumbura katika juhudi zao za kumzuia Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo. Hata hivyo alishiriki katika uchaguzi huo uliofanyika mwezi Julai na kupelekea kuongezeka machafuko ya umwagaji wa damu katika kona mbalimbali za Burundi. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, wanamgambo wa tawi la vijana la chama tawala cha CNDE-FDD walihusika katika mauaji ya kisiasa yaliyofanyika jijini Bujumbura. Wachambuzi hao wanasema kwamba, ni jambo lisilo na shaka kuwa vijana hao wa chama tawala wanahusika katika mauaji hayo hasa kwa kuzingatia kuwa, wakuu wa chama hicho ambacho kinaundwa na vyama vya baraza la taifa la kulinda demokrasia na harakati kwa ajili ya demokrasia walitaka Nkurunzinza abakie madarakani kwa hali yoyote ile. Wakati huo huo serikali ya Burundi inaituhumu Rwanda kuwa inafanya njama za kuchochea machafuko nchini humo. Kwa mara ya kwanza serikali ya Burundi imetoa ripoti ya kurasa 25 ya ushahidi wa kuhusika Rwanda katika machafuko ya Burundi. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuna uwezekano kwamba viongozi wa chama tawala cha CNDD-FDD wanajaribu kupunguza mashikizo yanayowakabili kupitia kuituhumu Rwanda kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Wakati duru mbalimbali zenye itibari zinawatuhumu vijana wa chama cha CNDD-FDD kuwa ndio wahusika wakuu wa uvunjaji wa haki za binadamu nchini Burundi, serikali ya Bujumbura inainyooshea kidole cha lawama nchi jirani ya Rwanda. Hata hivyo Rais Paul Kagame wa Rwanda amekanusha mara kadhaa kuhusika nchi yake katika machafuko ya Burundi. Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti ukiituhumu Rwanda kuwa inawasaidia waasi wa Burundi. Kwa upande wake serikali Burundi inadai kuwa Kigali inawapa mafunzo ya kijeshi wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda. Hata hivyo tuhuma zote hizo zimekanushwa vikali na serikali ya Kigali. Tukiweka pembeni tuhuma hizo, wananchi wa Burundi ndio wahanga wakuu wa machafuko ya nchi yao. Mbali na ukosefu wa usalama, wananchi hao wanateseka kwa mfumuko wa bei, kupanda maisha, njaa, ufisadi wa kiuchumi na mgogoro wa wakimbizi. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, njia bora ya kutatua matatizo ya Burundi ni kushirikiana nchi mbili za Rwanda na Burundi ambazo zina utamaduni wa pamoja, lugha yao ni moja na hata muundo wa watu wao ni mmoja badala ya kuzozana.