Homa ya Lassa imeshaua zaidi ya watu 100 nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i751-homa_ya_lassa_imeshaua_zaidi_ya_watu_100_nchini_nigeria
Maafisa wa kitengo cha Afya na Tiba nchini Nigeria wametangaza kuwa watu 101 wamefariki dunia kutokana na mripuko mpya wa homa ya Lassa uliotokea nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2016 04:00 UTC
  • Lassa fever in Nigeria
    Lassa fever in Nigeria

Maafisa wa kitengo cha Afya na Tiba nchini Nigeria wametangaza kuwa watu 101 wamefariki dunia kutokana na mripuko mpya wa homa ya Lassa uliotokea nchini humo.

Takwimu mpya zilizotolewa na Kituo cha Udhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC) aidha zinaonyesha kuwa mbali na watu 101 waliofariki tangu mwezi Agosti mwaka jana hadi sasa, jumla ya kesi 175 zimeripotiwa pia za watu waliothibitika au kushukiwa kuambukizwa kirusi cha ugonjwa huo.

Taarifa iliyotolewa na kituo hicho imeeleza kuwa hadi kufikia sasa maambukizi ya kirusi cha homa ya Lassa yameripotiwa katika mji mkuu wa kisiasa Abuja na ule wa kibiashara wa Lagos pamoja na majimbo mengine 14 ya nchi hiyo.

Wakati mamlaka za Afya nchini Ngeria zinaripoti kuwa kirusi cha Lassa kimeshadhibitiwa kuna hofu kwamba ukubwa halisi wa mripuko wa homa hiyo haujaripotiwa.

Mripuko wa homa ya Lassa nchini Nigeria ulitangazwa mwezi uliopita wa Januari miezi kadhaa baada ya kesi ya kwanza kushuhudiwa mnamo mwezi Agosti mwaka jana.

Kwa mujibu wa taasisi za kimataifa za udhibti magonjwa, kila mwaka watu kati laki moja hadi laki tatu hupatwa na homa ya Lassa huko Afrika Magharibi inayosababisha watu wapatao elfu tano miongoni mwao kupoteza maisha.

Homa ya Lassa iko katika jamii moja na maradhi ya Marburg na Ebola. Asili ya jina la ugonjwa huo ni mji wa Lassa ulioko kaskazini mwa Nigeria ambako ndiko ulikogundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1969.

Kirusi cha homa ya Lassa husambaa kwa kuchanganyika na chakula au vyombo vya ndani ya nyumba vinapochanganyika na choo kidogo au kinyesi cha panya au baada ya kuchanganyika na majimaji ya mwili wa mtu aliyepatwa na homa hiyo.../