Wanajeshi 22 wa serikali wauliwa na magaidi huko Sokoto, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75156-wanajeshi_22_wa_serikali_wauliwa_na_magaidi_huko_sokoto_nigeria
Watu wenye silaha wameua wanajeshi 22 wa serikali ya Nigeria katika shambulio baya kuwahi kutokea katika siku za hivi karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 28, 2021 08:16 UTC
  • Wanajeshi 22 wa serikali wauliwa na magaidi huko Sokoto, Nigeria

Watu wenye silaha wameua wanajeshi 22 wa serikali ya Nigeria katika shambulio baya kuwahi kutokea katika siku za hivi karibuni.

Radio Noor ya nchini Nigeria imeripoti habari hiyo na kutangaza kuwa, watu wenye silaha wameshambuia kituo kimoja cha kijeshi katika maeneo ya ndani kabisa ya mkoa wa Sokoto, kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuua wanajeshi 22 wa nchi hiyo.

Jumamosi iliyopita pia, kwa akali wanajeshi 20 wa Nigeria waliuawa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika baada ya kushambuliwa na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Maafisa wa jeshi la Nigeria waliziambia duru za habari kwamba, kwa akali wanajeshi 20 wa nchi hiyo wameuawa katika mapigano makali yaliyozuka baina yao na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Magaidi wa Boko Haram wanatumia hata wtoto wadogo kufanya jinai nchini Nigeria

 

Taarifa zaidi zilisema kuwa, mapigano hayo yalitokea katika eneo lililoko baina ya miji miwili ya Dikwa na Marte na kwamba, wanajeshi hao walishambuliwa ghafla walipokuwa njiani kuelekea mjini Maiduguri. Wanajeshi kadhaa pia waliripotiwa kujeruhiwa katika mapigano hayo.

Licha ya madai ya maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la Nigeria kwamba, jeshi la nchi hiyo linaelekea kuwashinda nguvu wanamgambo wa Boko Haram lakini katika majuma ya hivi karibuni, magaidi hao wameshadidisha hujuma na mashambulio yao dhidi ya wanajeshi na raia. Mamia ya wanajeshi wa Nigeria wameuawa na Boko Haram tangu mwezi Januari mwaka huu.