Maelfu waandamana Sudan; washinikiza utawala wa kiraia
(last modified Fri, 01 Oct 2021 07:44:25 GMT )
Oct 01, 2021 07:44 UTC
  • Maelfu waandamana Sudan; washinikiza utawala wa kiraia

Maelfu ya wananchi wa Sudan wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum dhidi ya watawala wa kijeshi na kushinikiza kuundwa uongozi mpya wa kipindi cha mpito ambao utawajumuisha pakubwa raia.

Waandamanaji hao huko Khartoum wamewatuhumu majenerali wa jeshi walioko madarakani hivi sasa kuwa wamechelewesha kipindi cha mpito kuelekea demokrasia. 

 Waandamanaji waliokuwa na hasira walipiga nara na shaari kama" jeshi ni jeshi la Sudan na si jeshi la Burhan, wakimnyooshea kidole Jenerali Abde Fattah al Burhan kiongozi wa baraza la utawala la Sudan. Maandamano mengi sawa na hayo ya Khartoum yameshuhudiwa pia katika miji mingine ya Sudan dhidi ya uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo. 

Abdul Fattah al Burhan, kiongozi wa baraza la utawala la Sudan

Sudan inaongozwa na serikali ya mpito inayosimamiwa na wanajeshi. Serikali hiyo iliasisiwa baada ya kung'olewa madarakani mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Miezi kadhaa baada ya al Bashir kuenguliwa madarakani, majenerali wanaoongoza kipindi cha mpito huko Sudan walikubaliana kugawana madaraka na raia. 

Maandamano hayo ya sasa nchini Sudan yaliyofanywa kufuatia jaribio la mapinduzi lililoshindwa wiki iliyopita yamedhihirisha migawanyiko ya waziwazi kati ya jeshi na makundi ya kiraia. 

Tags