Maiti 17 za wahajiri zapatikana ufukweni magharibi mwa Libya
Shirika la Hilali Nyekundu la Libya limesema maiti 17 za wahajiri wanaoaminika kufa maji baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuzama zimepatikana katika pwani ya magharibi ya nchi hiyo.
Shirika hilo limesema maiti hizo zilipatikana jana Jumanne karibu na mji wa magharibi wa Zawiya, na kwamba wahajiri hao wanasadikika kuwa walikuwa safirini kuelekea Ulaya.
Hilali Nyekundu ya Libya imesema miili ya wahajiri hao imekabidhiwa serikali kwa ajili ya shughuli za utambuzi na maziko. Huu unaonekana kuwa muendelezo wa matukio ya kufa maji wahajiri wakiwa katika safari hatarishi za kujaribu kuelekea Ulaya.
Kwa mujibu wa Shirika la Wahamiaji Duniani (IOM), wahamiaji haramu zaidi ya 1,100 wamekufa maji katika ajali za kupinduka boti zao hafifu baharini, tangu mwanzoni mwaka huu hadi sasa nchini Libya.
Libya inahesabiwa kuwa kitovu kikuu cha magendo ya wahajiri na wakimbizi wanaotaka kwenda nchi za Ulaya kutafuta ajira na kile wanachokitaja kuwa maisha mazuri.
Wiki iliyopita, serikali ya Libya ilianzisha msako mkali wa wahajiri haramu magharibi mwa nchi hiyo na kuwatia mbaroni wahajiri 4,000 wakiwemo mamia ya wanawake na watoto wadogo.