Wanavijiji 29 wengine wauliwa na watu wenye silaha nchini Nigeria
Taarifa za karibuni kutoka nchini Nigeria zinasema kuwa, watu 29 wengine wameuawa katika mashambulio ya watu wenye silaha kwenye maeneo ya kaskazini mashariki na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Duru za kieneo zimetangaza kuwa, watu hao 29 wameuawa katika jimbo la Zamfara la kaskazini mashariki na jimbo la Katsina la kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Duru hizo zimeongeza kuwa, watu wenye silaha wameshambulia kijiji kimoja katika eneo la msituni la Kawara kwenye jimbo la Zamfara na kuua watu 19 na kuchoma moto nyumba zao.
Watu hao wenye silaha wamewashambulia pia kwa risasi Waislamu waliokuwa wanarejea makwao kutoka msikitini katika jimbo la Katsina na kuua kwa umati Waislamu 10.
Mashambulizi ya umwagaji wa damu, ya kikabila na kidini yameongezeka nchini Nigeria hasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Machafuko hayo yameshapelekea karibu watu elfu mbili kuuawa, mamia ya wengine kujeruhiwa na maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao.
Magenge ya kigaidi yenye silaha nayo yanatumia vibaya mizozo hiyo ya kikabila na kikaumu, kufanya mashambulio dhidi ya raia, kuteka nyara watu hasa wanafunzi, kuvamia miji na vijiji, kuua raia wasio na ulinzi na kupora na kuchoma moto mali zao. hasa nyumba na mashamba.
Kushambuliwa na kuuliwa kwa umati Waislamu waliokuwa wanatoka Msikitini ni ushahidi wa wazi kuwa magaidi nchini Nigeria si Waislamu na hawajali matukufu ya kidini.