Nigeria yakomboa karibu mateka 200 kaskazini magharibi mwa nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75540-nigeria_yakomboa_karibu_mateka_200_kaskazini_magharibi_mwa_nchi_hiyo
Askari usalama wa Nigeria wamefanikiwa kuwakomboa karibu mateka 200 katika mashambulizi kadhaa yaliyofanyika dhidi ya kambi za magenge ya wahalifu katika msitu mkubwa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 08, 2021 23:58 UTC
  • Nigeria yakomboa karibu mateka 200 kaskazini magharibi mwa nchi hiyo

Askari usalama wa Nigeria wamefanikiwa kuwakomboa karibu mateka 200 katika mashambulizi kadhaa yaliyofanyika dhidi ya kambi za magenge ya wahalifu katika msitu mkubwa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

 Wahalifu hao waliojizatiti kwa silaha kwa miaka kadhaa sasa wamevamia maeneo ya kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria na mara kwa mara wamekuwa wakishambulia vijiji na kupora mali na kuwateka nyara wakazi wa vijiji hivyo huku wakitaka kupewa kikomboleo. 

Polisi katika jimbo la Zamfara nchini Nigeria imesema kuwa raia hao 187 waliokombolewa kutoka mikononi mwa magenge ya uhalifu ambao ni mchanganyiko wa   wanaume, wanawake na watoto, wamepelekwa katika jimbo la Zamfara ambako walitekwa nyara katika mashambulizi tofauti ya majambazi. Polisi imeoyesha picha za makumi ya wanaume, wanawake na watoto wakiwa wamekaa chini kwa kubanana baada ya kukombolewa.

Msemaji wa Polisi katika jimbo la Zamfara, Mohammed Shehu amesema kuwa raia hao ambao walikuwa mikononi mwa wahalifu hao kwa wiki kadhaa walikombolewa bila ya masharti yoyote Alhamisi hii kufuatia msako mkali na oparesheni za uokoaji zilizoendelea kwa masaa kadhaa. 

Visa vya kutekwa nyara raia vimekithiri sana nchini Nigeria katika miezi ya karibuni.

Jumanne iliyopita majambazi wasiopungua 100 waliokuwa kwenye pikipiki walizingira kijiji cha Kuryan Madaro katika jimbo la Zamfara na kuuwa watu 14. Wezi hao waliibia fedha na simu za raia. 

Magenge ya uhalifu Nigeria