Watu 20 wauawa katika shambulio la wabeba silaha nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75590-watu_20_wauawa_katika_shambulio_la_wabeba_silaha_nchini_nigeria
Watu wasiopungua 20 wameuawa katika shambulio la wabeba silaha huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Oct 10, 2021 04:20 UTC
  • Watu 20 wauawa katika shambulio la wabeba silaha nchini Nigeria

Watu wasiopungua 20 wameuawa katika shambulio la wabeba silaha huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu la Uturuki, watu wenye silaha jana Jumamosi walishambulia soko moja katika eneo la Sabon Birni kwenye jimbo la Sokoto na kuua watu 20.

Aidha watu wengine zaidi ya 35 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la watu wasiojulikana.

Haya yanajiri siku moja baada ya watu 11 akiwemo Imam kuuawa na genge la wabeba silaha la Yan Sakai lililoshambulia soko katika kijiji cha Mamande katika eneo la Gwadabawa.

Wabeba silaha nchini Nigeria

Jumanne iliyopita pia, majambazi wasiopungua 100 waliokuwa kwenye pikipiki walizingira kijiji cha Kuryan Madaro katika jimbo la Zamfara na kuuwa watu 14. Wezi hao waliibia fedha na simu za raia. 

Siku chache zilizopita pia, watu 29 wengine waliuawa katika mashambulio ya watu wenye silaha kwenye maeneo ya kaskazini mashariki na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.