Maafisa kadhaa wa Sudan wapigwa marufuku kutoka nje ya nchi
(last modified Wed, 13 Oct 2021 08:00:33 GMT )
Oct 13, 2021 08:00 UTC
  • Maafisa kadhaa wa Sudan wapigwa marufuku kutoka nje ya nchi

Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan Jenerali Abde Fattah el-Burhan amelitaka shirika kuu la intelijensia la nchi hiyo liwazuie maafisa kadhaa wa serikali wasisafiri kuelekea nje ya nchi.

Vyombo vya habari vimenakili duru moja ya kiusalama ya Sudan na kutangaza kuwa, miongoni mwa maafisa waliopigwa marufuku kufanya safari nje ya nchi ni Muhammad al Faki Suleiman, mjumbe wa baraza la utawala pamoja na wajumbe wengine kadhaa waandamizi wa kamati iliyovunjwa ya utawala wa rais aliyetangulia wa nchi hiyo Omar al Bashir.

Kuanzia Desemba 2018 Sudan iligeuzwa uwanja wa maandamano ya umma dhidi ya serikali ya al Bashir; na kufikia Aprili 2019 kiongozi huyo aling'olewa madarakani; na hivi sasa serikali ya mpito ndiyo inayoendesha masuala ya nchi.

Omar al Bashir

Katika miezi ya karibuni Sudan imeshuhudia vuta nikuvute za kisiasa na mapigano ya silaha katika maeneo kadhaa; ya karibuni kabisa yakiwa ni Darfur, magharibi mwa nchi na Kordofan ya kusini mwa nchi hiyo.

Kuleta suluhu na kurejesha amani, ni miongoni mwa masuala muhimu zaidi yaliyotangazwa kuwa yatashughulikiwa na serikali ya waziri mkuu Abdalla Hamdok katika uongozi wake wa mpito ulioanza Agosti 21 mwaka 2019. Serikali hiyo inatazamiwa kuongoza kwa muda wa miezi 39 na kuhitimisha kipindi chake cha uongozi kwa kuitishwa uchaguzi mkuu nchini humo.../

Tags