Israel yaingiwa na wasiwasi kuwa yamkini Sudan ikabatilisha mapatano ya ushusiano
(last modified Sat, 16 Oct 2021 07:15:53 GMT )
Oct 16, 2021 07:15 UTC
  • Israel yaingiwa na wasiwasi kuwa yamkini Sudan ikabatilisha mapatano ya ushusiano

Gazeti la Kizayuni la Maariv limefichua kuwa, wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel wana wasiwasi kuwa Sudan huenda ikajiondoa hatua kwa hatua katika mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo.

Hayo yamejiri baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan kutangaza Ijumaa kuwa nchi hiyo inapinga hatua ya mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika.

Kufuatia tangazo hilo, gazeti la Maarif limeandika kuwa, mapatano ya Tel Aviv na Khartoum ya kuanzisha uhusiano wa kawaida yaliyofikiwa siku za mwisho za utawala wa Donald Trump yalipaswa kuimarishwa kwa kutiwa saini mapatano ziada lakini hilo halijafanyika hadi sasa.

Aidha gazeti hilo la Kizayuni limeandika kuwa, wakuu wa Marekani wamekutana na maafisa wa serikali ya mpito ya Sudan kwa lengo la kuishinikiza Khartoum iimarishe uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Gazeti la Maariv limeandika kuwa Sudan iliondolewa na Marekani katika nchi zinazounga mkono ugaidi kwa sharti la kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Mariam Sadiq al Mahdi

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan alisema kuwa, miezi 11 tangu nchi yake itangaze kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel lakini hakuna ishara zozote za kuboreka uhusiano wa pande mbili kama ambavyo hakuna pia mazungumzo yoyote rasmi yaliyofanyika baina yazo.

Bi Mariam Sadiq al Mahdi amesema hayo katika mahojiano na gazeti la National la Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kuongeza kuwa, kufutwa sheria ya vikwazo dhidi ya Israel hakuna maana ya kuruhusu kufunguliwa ubalozi wa Israel mjini Khartoum.

Tags