Nov 05, 2021 07:47 UTC
  • Wakimbizi 15,000 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wamiminika Kongo DR

Zaidi ya raia 15,000 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliokimbia mapigano kati ya jeshi na waasi wamevuka mpaka na kuingia eneo la Bosobolo, Ubangi Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndani ya muda wa siku 17.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na afisa wa eneo hilo ambaye ameomba msaada kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada na mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jeannot Haolo amevieleza vyombo vya habari: "kwa jumla, wakimbizi 15,059 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, wanawake 1,637 na watoto 11,892, wamefika katika eneo la Bosobolo huko Ubangi Kaskazini, kulingana na takwimu zilizotolewa na Idara ya Uhamiaji ya Kongo DR."

Haolo ameongeza kuwa, watu hao walianza kutoroka nchi yao kati ya Oktoba 10 na 27, yaani katika muda wa siku 17.

Raia hao kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakimbia mapigano kati ya vikosi tiifu, vinavyosonga mbele, na waasi wa makundi ya Seleka na Anti-Balaka.

Waasi wa Kikristo wa Anti Balaka Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kwa mujibu wa afisa huyo, mapigano ya hivi karibuni yalitokea karibu na mji wa Kouango nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Eneo la Bosobolo liko katika jimbo la Nord-Ubangi kaskazini-magharibi mwa Kongo DR kwenye mpaka wa pamoja na CAR.

Kulingana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, kuna jumla ya wakimbizi 221,694 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini Kongo DR. 114,008 wamepewa hifadhi huko Nord-Ubangi.

Ripoti zinasema, mwezi uliopita wa Oktoba, wakimbizi 250 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati walirejeshwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.../

 

Tags