Dec 24, 2023 07:10 UTC
  • Jamhuri ya Afrika ya Kati yapinga azma ya Marekani ya kutuma silaha nchini humo

Jamhuri ya Afrika ya Kati imelaani hatua ya Marekani ya kutaka kupeleka zana za kijeshi nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Sylvie Baïpo-Temon, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, amesema kuwa hakuwa na habari kuhusiana na azma ya Marekani ya kupeleka silaha na vifaa vyake vya mawasiliano ya kijeshi katika nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema hatua hiyo kwa mara nyingine tena inaonyesha siasa za kundumakuwili za Baraza la Usalama.

Sylvie Baipo-Temon amebainisha kuwa Marekani imelijulisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu azma yake ya kupeleka silaha na zana za mawasiliano ya redio katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa ni sehemu ya operesheni zake kadhaa za kijeshi nchini humo.

Amesisitiza kuwa kwa kawaida ni nchi inayohitajia jambo au msaada fulani ndiyo hutoa ombi la kukidhiwa mahitaji yake na sio nchi nyingine kuichukulia maamuzi ya vitu itakavyotuma katika nchi inayolengwa. Amesema, Jamhuri ya Afrika ya Kati ni nchi huru inayopasa kujichukulia maamuzi kwa msingi wa maslahi yake ya kitaifa. Amesisitiza kuwa mtu yeyote anayetaka kufanya jambo lolote katika nchi hiyo anapasa kushirikiana na kuwashauri viongozi wake.

Tags