Jun 10, 2023 11:22 UTC
  • Ukatili wa kingono CAR; UN kuwatimua askari 60 wa Tanzania

Umoja wa Mataifa umesema utawafukuza makumi ya askari wa Tanzania, ambao ni sehemu ya Kikosi cha Kulinda Amani cha moja huo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) kwa kutuhumiwa kufanya unyanyasaji wa kingono.

Msemaji wa UN, Stephane Dujarric amesema uchunguzi wa awali umekusanya ushahidi wenye mashiko, unaoonyesha kuwa wanajeshi 11 wa Tanzania ambao walikuwa sehemu ya kikosi cha askari 60 wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki huko magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliwafanyia dhulma za kingono watu wanne.

Amesema Umoja wa Mataifa ulifanya uchunguzi wa ndani kutathmini tuhuma hizo, kuwatambua na kuwasikiliza wanaodaiwa kuwa waathiriwa wa vitendo hivyo viovu.

Umoja wa Mataifa umesema tayari umeziarifu mamlaka za Tanzania kuhusu tuhuma hizo dhidi ya askari wake wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Serikali ya Dar es Salaam imesema imetuma timu ya uchunguzi CAR kwenda kufuatilia kadhia hiyo.

Msemaji wa UN, Stephane Dujarric

UN imekuwa ikitoa ripoti mara kwa mara, zinazoonyesha kuongezeka kwa matukio ya vitendo viovu vya kingono vya askari wa Kofia Buluu katika sehemu mbalimbali duniani hasa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Mataifa umetuma maelfu ya wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati maarufu kwa jina la MINUSCA tokea mwaka 2014.

Tags