Mgodi wa dhahabu waporomoko na kuua watu 85 nchini Nigeria
Makumi ya wachimba migodi wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu nchini Nigeria.
Zahra'addin Sirajo, mwandishi wa habari katika jimbo la Katsina ameliambia shirika la habari la Iran Press kuwa, miili 85 imepatikana katika mgodi wa dhahabu katika kijiji cha Kwandago, umbali wa kilomita 15 kutoka Danisa, mji ulioko katika mpaka wa Nigeria na Niger.
Serikali za Niger na Nigeria hazijatoa taarifa kuhusu maporomoko hayo yaliyotokea katika timbo la dhahabu, usiku wa kuamkia leo Jumanne.
Mamia ya wananchi wa nchi mbili hizo jirani za Afrika Magharibi hufurika kwenye migodi ya dhahabu inayopatikana katika kijiji cha mpakani cha Kwandago.
Kabla ya hapo, wachimba migodi 18 waliripotiwa kufariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu kusini mwa Niger, mpakani na Nigeria.
Adamou Gueraou, meya wa wilaya ya Dan-Issa amesema wachimba migodi hao walioaga dunia walizikwa jana Jumatatu, na kwamba majeruhi saba wa mkasa huo wamelazwa hospitalini.
Habari zaidi zinasema kuwa, ajali hiyo ilitokea juzi Jumapili katika timbo la Garin-Liman, linalopatikana katika jimbo la Maradi, kusini mwa nchi.
Takwimu zinaonyesha, aghalabu ya madini hususan ya dhahabu yanayochimbwa kinyume cha sheria nchini Nigeria, Niger pamoja na nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.