Watu watatu wafariki dunia nchini Kenya katika maandamano ya wapinzani wa serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7693-watu_watatu_wafariki_dunia_nchini_kenya_katika_maandamano_ya_wapinzani_wa_serikali
Watu watatu wamepoteza maisha yao na wengine kadhaa kujeruhiwa nchini Kenya baada ya maandamano ya mrengo wa upinzani ya kutaka Tume ya Uchaguzi na Mipaka IEBC ijiuzulu kugeuka na kuwa uwanja wa fujo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2016 23:12 UTC
  • Watu watatu wafariki dunia nchini Kenya katika maandamano ya wapinzani wa serikali

Watu watatu wamepoteza maisha yao na wengine kadhaa kujeruhiwa nchini Kenya baada ya maandamano ya mrengo wa upinzani ya kutaka Tume ya Uchaguzi na Mipaka IEBC ijiuzulu kugeuka na kuwa uwanja wa fujo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mtu wa kwanza alifariki dunia huko Kisumu huku wawili wakipoteza maisha yao katika Kaunti ya Siaya baada ya maandamano ya mrengo wa upinzani kugeuka na kuwa uwanja wa machafuko hapo jana. Polisi ililazimika kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao. Taarifa zaidi zinasema kuwa, kuna uwezekano wa idadi ya vifo kuongezeka kutokana na watu kadhaa kujeruhiwa vibaya katika Kaunti ya Siaya. Madaktari waliomtibu mtu wa kwanza aliyeaga dunia wamethibitisha kuwa, marehemu hakuaga dunia kutokana na majeraha ya risasi. Machafuko yalizuka katika mji wa Kakamega baada ya makundi mawili moja likiwa linaunga mkono maandamano hayo na la pili likipinga, kukabiliana na kusababisha watu wengi kujeruhiwa. Moses Wetangula mmoja wa viongozi waandamizi wa mrengo wa upinzani nchini Kenya amelaani vikali hatua ya vikosi vya usalama kutumia nguvu za ziada dhidi ya waandamanaji. Maandamano ya wapinzani nchini Kenya hufanyika kila Jumatatu kwa lengo la kushinikiza kujiuzulu makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC. Wapinzani nchini humo wanashinikiza kujiuzulu wakuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka wakisisitiza kuwa hawana imani nao na kwamba, tayari wamekula njama na serikali ili kufanya uchakachuaji katika uchaguzi mkuu ujao, wa Agosti mwakani. Hata hivyo serikali ya Jubilee imewataka viongozi wa upinzani kutumia taratibu za kisheria na miongozo ya katiba ili kuwaondoa ofisini makamishna wa tume ya uchaguzi.