Askari walinda amani 28 wa UN wameuawa mwaka huu nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78144-askari_walinda_amani_28_wa_un_wameuawa_mwaka_huu_nchini_mali
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, askari wake walinda amani 28 wameuawa na wengine 165 wamejeruhiwa nchini Mali katika mwaka huu unaomalizika wa 2021.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 17, 2021 23:10 UTC
  • Askari walinda amani 28 wa UN wameuawa mwaka huu nchini Mali

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, askari wake walinda amani 28 wameuawa na wengine 165 wamejeruhiwa nchini Mali katika mwaka huu unaomalizika wa 2021.

Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa amevieleza vyombo vya habari kuwa, akthari ya walinda amani hao wameuawa au kujeruhiwa kwa miripuko ya mabomu ya kutengeneza kwa mkono.

Hayo yamejiri katika hali ambayo katika kipindi chote cha mwaka huu, askari wa kulinda amani wa UN wanaohudumu chini ya mpango wa umoja huo nchini Mali unaojulikana kama MINUSMA wametekeleza jumla ya operesheni 13,000 za doria na 100 za kulinda usalama wa raia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Tarehe 8 Desemba, askari saba walinda amani waliuawa na wengine watatu walijeruhiwa baada ya msafara wao wa magari yaliyobeba vifaa vya huduma kukanyaga bomu katika mji wa Bandiagara uliopo mkoani Mopti kaskazini mwa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2012, Mali imekuwa ikishuhudia mapinduzi ya kijeshi na machafuko ya ndani baada ya makundi ya kigaidi kupata nguvu nchini humo.

Walinda amani wa MINUSMA na askari wa Ufaransa wamekuwepo nchini Mali kuanzia katikati ya mwaka 2013, lakini hawajafanikiwa kurejesha uthabiti kwa kiwango cha kuridhisha na hadi sasa vitisho vya ugaidi vingali vinaendelea kuiandama nchi hiyo.../