Kuendelea mgogoro nchini Sudan sambamba na kukandamizwa wapinzani
(last modified Tue, 21 Dec 2021 09:35:11 GMT )
Dec 21, 2021 09:35 UTC
  • Kuendelea mgogoro nchini Sudan sambamba na kukandamizwa wapinzani

Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ungali unaendelea. Akthari ya raia wa Sudan wameendelea kujitokeza katika barabara na mitaa ya miji mbalimbali ya nchi hiyo wakionyesha upinzani wao dhidi ya utawala wa kijeshi na kusisitiza kueendeleza maandamano hadi demokrasia itakapochukua mkondo wake.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu wamesikika wakipiga nara za kutaka raia kuwa nafasi katika uongozi na utawala wa kiraia kushika hatamu za uongozi wa nchi.

Hii ni katika hali ambayo, maandamano na mkusanyiko wa wananchi wa Sudan mbele ya vikosi vya kijeshi uligeuka na kuwa uwanja wa utumiaji mabavu. Polisi walifyatua mabomu ya gesi ya kutoa machozi na hata risasi hai. Ripoti ya Wizara ya Afya ya Sudan inaeleza kuwa, zaidi ya waandamanaji 121 walijeruhiwa katika sokomoko hilo. Kwa upande wake, Kamati ya Madaktari wa Sudan imetoa taarifa ikieleza kwamba, kwa kali watu 43 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa tangu Oktoba 25 mwaka huu wakati jeshi la Sudan lilipofanya mapinduzi na kuhodhi madaraka ya nchi.

 Maandamano ya wapinzani nchini Sudan yanafanyika katika hali ambayo, kwa muda sasa nchi hiyo imekuwa ikisakamwa na mgogoro wa kisiasa. Kutokea mapinduzi laini ya kijeshi kumeongeza malalamiko na maandamano ya wananchi. Licha ya jeshi kusalimu amri na kulazimika kumrejesha tena madarakani Waziri Mkuu Abdalla Hamdok, lakini hatua hiyo haijatuliza munkari na hasira za wananchi. Wananchi wa Sudan ambao miaka mitatu iliyopita waliiondoa madaraka serikali ya muda mrefu wa Omar Hassan al-Bashir kupitia vuguvugu na maandamano yao, filihali wanahisi kwamba, malengo yao ya kufanya mapinduzi yapo hatarini.

Abdalla Hamdok Waziri Mkuu wa Sudan

 

Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu Hamdok anasema kuwa, amerejea katika nafasi hiyo ili kuzuia kumwagika zaidi damu na kutosambaratika matunda yaliyopatikana hapo kabla kupitia mapinduzi ya wananchi. Pamoja na hayo Wasudan wametangaza kuwa, wanajeshi wanapaswa kukaa kando kikamilifu katika uongozi na kwamba, makubaliano yao ya kisiasa na Hamdok ni kitu kisichokubalika.

Ashraf Abdul-Aziz, Mhariri Mkuu wa gazeti huru la al-Jaridah anasema kuhusiana na hilo: Mapinduzi yamekuwa kizingiti katika njia ya kukabidhi madaraka kwa njia ya demokrasia na kulipatia jeshi fursa ya kuwa na udhibiti kikamilifu kwa siasa na uchumi. Kwa sasa vyombo vya usalama vina udhibiti kamili wa asasi za kisiasa za nchi hiyo.

Abdalla Hamdok sanjari na kutoa indhari kwamba, Sudan imeikengeuka mno njia ya mapinduzi yake amesisitiza kuwa, ukengeukaji huo ni tishio kwa usalama, umoja na uthabiti wa nchi. Hamdok ameeleza bayana kwamba: "Hii ni indhari ya kuanza uporomokaji wa maangamizi ambayo hayatatubakishia nchi wala mapinduzi."

Hivi sasa viongozi wa Sudan wanafanya juhudi za kutuliza malalamiko na maandamano ya wananchi kupitia ahadi ya kuitisha uchaguzi. Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kamanda wa jeshi aliyeongoza mapinduzi ambaye kwa sasa ndio Kiongozi wa Baraza la Utawala amesisitiza kuwa, atafanya juhudi ili kutekelezwe matakwa ya mapinduzi na kuundwa serikali ya kiraia iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia mwishoni mwa kipindi cha mpito sambamba na kufanya hima ya kuondoa hitilafu na kuleta umoja wa Wasudan. Pamoja na hayo, wananchi wa Sudan wanachotaka ni kuitishwa uchaguzi huru na kuwekwa kando ya ulingo wa kisiasa wanajeshi wa nchi hiyo.

 

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kamanda wa jeshi aliyeongoza mapinduzi ambaye kwa sasa ndio Kiongozi wa Baraza la Utawala

Katika mazingira kama haya, uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya Sudan umeshadidisha mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Baadhi ya madola ya Magharibi na majirani wa Sudan wamekuwa wakitoa himaya ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja kwa majerali wa jeshi hatua ambayo kivitendo inalenga kudhamini maslahi yao.

Alaa kulli haal, katika hali ya sasa Sudan ina njia mbili kwa ajili ya kuainisha mustakabali wake. Kwa upande mmoja inapaswa kuukubali utawala wa kijeshi ambapo kwa mujibu wa akthari ya wananchi wa nchi hiyo hakutakuwa na jingine katika hilo ghairi ya tajiriba kama ile ya kipindi cha utawala wa Omar al-Bashir. Ama kwa upande wa pili, hakuna budi isipokuwa kuendeleza mapambano mpaka kuwadie kipindi cha kufanyika uchaguzi huru na kuundwa serikali ya kiraia. Ishara zote zinaonyesha kuwa, Wasudan wameamua kuichagua njia ya pili. 

Tags